Subscribe Us

Header Ads

Watu 16 wauawa katika shambulizi la anga katika shule ya Gaza


Takriban watu 16 wameuawa katika shambulizi la anga la Israel kwenye shule moja katika Ukanda wa Gaza, maafisa wa Palestina wamesema. Makumi ya wengine wamejeruhiwa.

Jengo hilo lilikuwa likihifadhi maelfu ya watu waliokimbia makazi yao katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat katikati mwa Gaza, kulingana na wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas.

Kikosi cha Ulinzi cha Israel (IDF) kilisema kiliwashambulia "magaidi kadhaa waliokuwa wakiendesha shughuli zao katika majengo yaliyo katika eneo la Shule ya Al-Jaouni".

Wakati huo huo, kumekuwa na ripoti kwamba watu 10 waliuawa katika shambulio tofauti la anga kwenye nyumba katika kambi hiyo.

Video kutoka eneo la shambulizi la shule ya Nuseirat inawaonyesha watu wazima na watoto wakipiga kelele katika barabara iliyojaa moshi na vumbi na vifusi, huku wakikimbia kusaidia majeruhi.

Watu walioshuhudia tukio hilo waliambia BBC kwamba shambulio hilo lililenga orofa za juu za shule hiyo, ambayo iko karibu na soko lenye shughuli nyingi.

BBC inaelewa kuwa hadi watu 7,000 walikuwa wakitumia jengo hilo kama makazi.

Mwanamke mmoja aliambia shirika la habari la AFP jinsi baadhi ya watoto walivyouawa walipokuwa wakisoma Quran wakati jengo liliposhambuliwa.

"Hii ni mara ya nne wanalenga shule bila kutoa onyo," alisema.

Chanzo cha ndani kilisema lengo lilikuwa chumba kinachodaiwa kutumiwa na polisi wa Hamas. Hata hivyo, BBC haiwezi kuthibitisha dai hili.

Hamas ilisema waandishi wa habari watano wa ndani ni miongoni mwa waliouawa katika mashambulizi ya Israel siku ya Jumamosi. Wanafamilia yao pia waliripotiwa kulengwa.

Zaidi ya waandishi wa habari 100 wamepoteza maisha huko Gaza tangu mashambulizi ya Oktoba 7, kulingana na Waandishi Wasio na Mipaka.

Hamas ilisema vifo vitano vya hivi punde vinafanya idadi hiyo kufikia 158.

.
Maelezo ya picha,Takriban watu 50 walijeruhiwa katika shambulizi hilo, maafisa wa Gaza wanasema.

Katika taarifa iliyotumwa kwenye mtandao wa X - ambao zamani ulijulikana kama Twitter - IDF ilithibitisha kushambulia majengo ya shule, ikisema kuwa imechukua "hatua nyingi" "kupunguza hatari ya kuwadhuru raia, ikiwa ni pamoja na matumizi ya uchunguzi sahihi wa angani na intelijensia ya ziada" .

Wanamgambo wa Hamas walikuwa wakitumia eneo hilo kama "maficho" kufanya mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa IDF, ilisema.

"Hamas inaendelea kukiuka sheria za kimataifa kwa kutumia vibaya miundo ya kiraia na raia kama ngao kwa mashambulizi yake ya kigaidi dhidi ya Taifa la Israel," iliongeza.

Hamas imeliita shambulizi hilo kama "mauaji" dhidi ya "raia wasio na ulinzi".

Wengi wa waliofariki na kujeruhiwa walikuwa wanawake, watoto na wazee, kundi hilo lilidai kupitia chaneli yake ya Telegram ya lugha ya Kiingereza.

Soma zaidi: